Jumanne, 31 Mei 2022

JINSI YA KUISHI NA WATU WAGUMU KUELEWA OFISINI, NA KATIKA MAHUSIANO.


Kuishi na watu wagumu kuelewa ni kazi sana hasa ukiwa mtu wa hasira za karibu au muoga wa kukosolewa.


Leo tuzungumzie kuhusu aina hii ya watu ambao huwa watata sana,wagumu kukubali makosa, wakosoaji sana wa tabia za wengine n.k ujue namna ya kuishi nao.

Huenda ni mzazi,mwajiri wako mfanyakazi wako,ndugu yako wa damu au rafiki yako ambaye kwa tabia zake mnakuwa na ugomvi kila wakati,unaogopa kuzungumza nae kwa sababu mtapishana mawazo muda wote 

Leo fahamu akili zao zipoje na namna ya kuishi nao.

Anaweza kuonekana mtu wa maadili sana, misimamo mikali sana, sheria ngumu sana,hataki ushauri akifanya maamuzi,haamini kama watu wengine wanaweza kufanya kazi bila usimamizi.

Wapo na misimamo 12 kama ifuatavyo

1.Hutaka matokeo kuwa kwa kiwango cha 100%, kazi yoyote ambayo itakuwa na dosari hata moja inakuwa haifai.Hawezi kufurahia kazi ya mtu yeyote isipokuwa ifikie viwango vyake tu 

2.Anakuwa na sheria ngumu, misimamo mikali sana,hataki masihara,hana huruma,yupo na kanuni ambazo hataki zivunjwe.Anaweza kukataa vitu kwa sababu tu sheria zake zimekiukwa 

3.Anakuwa na hofu sana,anaweza kuahirisha kazi kwa sababu ya kuepuka kufanya makosa,hurekebisha sana kazi na tabia za watu mpaka anakuwa na maadui wengi 

4.Huwa anataka kudhibiti pesa,ratiba,na taarifa zote muhimu zinakuwa chini yake na hataki mtu yeyote kuingilia maamuzi hayo.anataka taarifa muhimu za watu wake wa karibu ziwe chini yake,

anataka kumpangia kila mtu namna ya kuishi ,kutumia pesa,masomo gani yanafaa,

kuchagulia watu biashara na kazi za kufanya kwa kile anaita yupo na uzoefu na anajua sana kuliko wao 

5.Anaweka viwango vya juu sana vya mafanikio kwa kila mtu.Anaweza kumpangia ufaulu mtoto wake na kumlazimisha afikie ufaulu huo tofauti na hivyo anakuwa amefeli.

Anaweza kumlaumu mtoto kwa kupata 98% badala ya kupata 100% kwenye masomo,anaweza kumfokea mtoto wake kwa kushika namba 2 darasani badala ya namba moja bila kujali ugumu wa masomo au afya ya mtoto 

6.Hufanya sana kazi mpaka hukosa muda wa kujumuika na marafiki,ndugu na familia.

7.Hawezi kubadili mtazamo wake,akisema mawasiliano yake na watu  wengine ni njia ya simu labda kuongea tu sms hajibu hata kama muda upo

8.Yupo sahihi muda wote,hana makosa,ni mkamilifu siku zote na makosa yapo kwa wengine.

9.Anakuwa na hasira na misimamo mikali kuhusu pesa,muda,na anataka kila kitu kiende vile amepanga yeye 

10.Hawezi kuwapa kazi watu wengine kusimamia,anataka kazi zote afanye yeye, haamini watu wengine hivyo kazi zote anataka kufanya na kuzisimamia,akikupa kazi ikiwa na dosari hata moja utapewa lawama na kukosolewa sana  

11. Anapata wakati mgumu sana kuruhusu  pesa au mali kwenda kwa mtu mwengine

12.Huwa na kanuni ngumu sana kuhusu maadili,anaweza kuhukumu vitu kwa njia mbili tu kizuri na kibaya tu hakuna kati na kati ,hana uwezo wa kuonyesha huruma ,ukiwa nae anakuwa baridi sana kama hana hisia zozote kwako 

MAISHA YA MAHUSIANO YAO

Kwenye mapenzi hawana hisia za mapenzi kwa kuonyesha tabasamu,kujali, kubembeleza,kuwa romantic hawawezi,wao huona huo ni utoto na kupoteza muda 

Anaweza kuvaa vizuri sana,anaweza kuwa na lugha ya maadili sana muda wote, anaonekana kujiamini sana , mchapakazi hodari sana.

Mahusiano yake ni kufoka, kulaumu, kukosoa sana kila kitu cha mwenza wake ,anaweza kuwa havuti sigara wala hatumii pombe ila hana hisia za upendo kwako , haonyeshi kuhitaji msaada wako zaidi ya kukupa maagizo

Huwa watu wa kufuata ratiba muda wote,ukiishi nae muda wote kuna ratiba ya kila kitu na ukifanya tofauti na ratiba utafokewa sana na kukosolewa

Huwa waaminifu sio  rahisi kusaliti mahusiano yao ila ukiwa nae muda wote unatakiwa kufuata sheria,mpaka kwenye mapenzi anataka vifungu vya sheria

Kuna tabia anataka kuziona kwako na siku zote ugomvi utaibuka kwa sababu utashindwa kufikia viwango vyake 

Kama umezaliwa na mzazi mwenye hasira sana,mlevi kupindukia, mkorofi sana,mgonjwa sana au mzee sana au mtu wa maadili sana tena yenye sheria ngumu sana utajikuta unampata mwenza wa aina hii

Wao huvutiwa sana na watu ambao wao huwaona kama hawajafikia viwango fulani vya maadili ili wapate nafasi ya kuwa-control 

Watu wa aina hii hutafuta watu ambao wao wanaona itakuwa rahisi kuwa-control na kuwapangia kila kitu ,hupenda kutoa ushauri bila kuulizwa.

Anaweza kuvutiwa na mtu anaempenda sana starehe kisha wao wanataka kumkataza kufanya starehe ,au kutafuta mtu mvivu sana ili waanze kumfundisha nidhamu 

Anaweza kuvutiwa na mtu asiependa maadili ili wao waanze kumfundisha maadili

HAWANA FURAHA KWAKO

Ukiwa na mtu wa aina hii sana sana utasikia vifungu vya maandiko muda wote,hupati nafasi ya kuzungumza zaidi utakuwa unafundishwa muda wote

Hawana uwezo wa kuvutiwa na mtu ambaye anajisimamia kimaadili kwa sababu watakuwa na mvutano wa migogoro mara kwa mara

Ukiwa nae faraghani hawezi kusema anakupenda,ukimuuliza kama unanipenda atasema "kama sikupendi nisingekuwa hapa" 

KUKOSOLEWA

Hii inakuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku,anaweza kuwa na malengo makubwa na anataka uwe na malengo kama yake na mtazamo kama wake na vipaumbele kama vyake tofauti na hivyo hufai 

Kwa mfano anaweza kukosoa uvaaji,chakula, kutandika kitanda,kufua,kupanga viatu kwenye shoe rack,kukosoa upishi,kukosoa matumizi ya umeme,kukosoa usafi na mpangilio wa vitu vya ndani 

Huwezi kufanya chochote ambacho yeye ataona kimefikia viwango vyake 

Siku zote atarekebisha tabia zako mpaka ukimuona utaanza kuondoka kabla hajafika kwako 

HUOGOPA MAHUSIANO YA KARIBU SANA

Hawataki uwe romantic,atakosoa sana ukiwa mtu wa romance,akiona unataka kuwa karibu sana atapunguza muda wa kukaa na wewe 

KAMA MZAZI 

Sehemu kubwa ya malezi ni kukosoa, kurekebisha tabia na kuonyesha makosa ya watoto 

Ukifanya vizuri anakaa kimya, ukifanya makosa anaongea 

Hali hii hufanya  mtoto kuishi kwa hofu ya kukosolewa,kutajwa makosa yake 

Anataka mtoto asome kile amesoma,awe na vipaumbele kama vyake,hataki mtoto kufanya kazi tofauti na ile anafanya yeye au kusoma masomo tofauti na yake 

KAZINI

Huwa mabingwa wa kufanya kazi sana kuliko mtu yeyote.Hujituma sana na kufanya kazi vizuri sana

Huepuka makosa na mapungufu katika kazi zao 

Hawana masihara kazini

Ni wagumu kubadilika kuendana na mabadiliko ya mazingira.

Hukosoa sana kazi za wengine hasa ambao wapo chini yao 

Hutaka kufanya kazi zote wao tu.

MAGONJWA YAO 

Husumbuliwa msongo wa mawazo kwa sababu ya   hasira sana,hupata magonjwa ya moyo, kisukari, madonda tumbo, uvimbe,uzito kupita kiasi,stroke,kinga ya mwili kushuka na huwa hatarini kupata saratani,magonjwa ya bakteria na virusi haraka kuliko wengine

Maumivu ya kichwa, mgongo, uchovu,kuishiwa nguvu,

Sehemu kubwa ya magonjwa yao huwa ambayo sio ya kuambukiza kwa sababu ya hasira na "stress" kupita kiasi.



0 Comments:

Chapisha Maoni