Hadithi Ya Kustahili Kusikilizwa
Hao zamani za kale, ndege watatu walijenga viota vyao katika mti wa maembe karibu na nyumba ya mzee mmoja. Siku moja, mzee huyo alifika na shoka mkononi, akikusudia kuukata mti huo. Ndege wale waliingiwa na hofu, wakaanza kuomba kwa machozi na sauti za huzuni.
Ndege wa kwanza alisema,
"Tafadhali, usikate mti huu bado. Tupe wiki moja tu ili tuangue mayai yetu. Tafadhali, ewe mzee mwema!"
Ndege wa pili akaunga mkono,
"Ndiyo, anachosema ni kweli. Hatukukatazi kuukata mti huu, bali tunaomba tu utupe muda wa wiki moja, ili vifaranga wetu wawe wameanguliwa. Tafadhali, wiki moja tu!"
Ndege wa tatu akasema kwa uchungu,
"Mimi nimekuwa tasa kwa miaka mingi, hadi Mungu aliponibariki na mayai haya. Sitaki kupoteza nafasi hii ya kuwa mama. Sote watatu tunakuomba, tupe siku chache tu za kutulia hapa. Tafadhali, usikate mti huu bado!"
Lakini licha ya maombi yao, mzee alinguruma kwa hasira,
"Hapana! Lazima nikate mti huu sasa hivi! Sijali mnachosema! Nitafumba macho, na nikiyafumbua bado mpo hapa... ah, nitawaweka wote kwenye sufuria yangu ya supu!"
Waliposikia hayo, ndege wale waliogopa sana. Kwa haraka wakapaa na kuruka mbali kuokoa maisha yao—hawakurudi tena.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye, ndege wa tatu alirudi kwenye mti. Mzee akashangaa sana, akamuuliza kwa hasira,
"Nilidhani mmekimbia wote! Kwa nini umerudi?"
Ndege huyo alipiga filimbi kisha akasema kwa utulivu,
"Mimi sikuikimbia hatari. Nilienda tu kuleta mboga na viungo vya kupikia ili ukishaniua, viwe vya kukutia ladha supuni. Kama unadhani nitaacha mayai yangu, nafasi yangu pekee ya kuwa mama... umekosea sana."
Mzee alinyamaza kwa muda mrefu. Moyo wake ukalainika kwa mshangao na huruma. Kisha akasema kwa sauti ya upole,
"Wewe ni jasiri sana. Kwa ajili ya ujasiri wako, nakupa heshima yangu. Nitakupa muda mrefu wa kutosha kuangua mayai yako na kulea vifaranga wako kabla sijakata mti huu. Wale ndege wengine wawili... wao ni waoga tu!"
Ujasiri siyo kukosa hofu, bali ni kuchukua hatua hata ukiwa na hofu.
Sote hujisikie kutishiwa na kukatishwa tamaa wakati mwingine. Watu wanaweza kukutishia makusudi, lakini usikubali kutishwa. Usikimbie haraka. Simama imara. Kuwa jasiri. Kwa sababu vitisho vingi ni maneno tu, visivyokuwa na nguvu ya kweli.
Kuwa jasiri. Kuwa imara. Usihofu.

0 Comments:
Chapisha Maoni