Habari za wakati huu. Mimi ni Roghat Falme Robert, Mwanzilishi wa Akili Platform Tanzania, shirika lilojikita katika afya ya akili, mazingira na haki za binadamu. Leo tunatoa mtazamo wetu kuelekea Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani, siku muhimu inayotukumbusha dhamana yetu ya kuhakikisha jamii inakuwa jumuishi na yenye usawa kwa watu wote.
Kwa watu wenye ulemavu, siku hii ni zaidi ya maadhimisho; ni nafasi ya kuthibitisha uwezo wao, kupaza sauti juu ya changamoto wanazokutana nazo, na kuhimiza kutambuliwa kwa haki zao. Mara nyingi huiona kama siku inayojenga matumaini, umoja na faraja kutokana na kuonekana na kusikilizwa katika ngazi za kijamii na kitaifa.
Kwa upande wa jamii, siku hii ni mwaliko wa kuimarisha uelewa na kubadili mtazamo. Ni siku ambayo jamii inahimizwa kuvunja dhana ya luweka majina kandamizi kama kipofu,Chizi,Mtambo, Mbumbumbuu,Chenga na dahana zote potofu, kuondoa ubaguzi na kuhakikisha kuwa mazingira yote—shuleni, kazini, mitaani na ndani ya familia—yanakuwa rafiki na yenye fursa sawa kwa watu wenye ulemavu bila kisingizio cha aina yoyote.
Kwa upande wa ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia, Akili Platform Tanzania tunaona umuhimu wa kuwepo kwa fursa maalumu zinazowalinda watu wenye ulemavu, hususan wanawake na watoto. Hii inajumuisha mafunzo ya haki na usalama, vituo rafiki vya kuripoti ukatili, huduma za afya ya uzazi zisizo na vikwazo, msaada wa kisheria, na uwezeshaji kiuchumi unaopunguza utegemezi unaowafanya kuwa hatarini kukumbana na unyanyasaji.
Tunaiomba jamii iwajumuishe watu wenye ulemavu kikamilifu katika shughuli zote za kijamii na kiuchumi. Ni muhimu tuondoe vikwazo vya kimazingira, tuweke mifumo rafiki kwa wote, na tuwatendee kwa heshima na utu bila kuwatenga au kuwaona kama watu wasioweza. Ulemavu si udhaifu—ni sehemu ya utofauti wa binadamu, na kila mmoja ana mchango halisi katika maendeleo ya taifa letu.
Kwa niaba ya Akili Platform Tanzania, tunasisitiza kuwa kujenga jamii jumuishi ni wajibu wa kila mmoja. Tunaendelea kufanya kazi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata nafasi sawa, huduma stahiki na ulinzi wa kutosha.
Tukiimarisha ushirikishwaji, tunajenga taifa lenye haki, usawa na utu kwa wote hasa wenye ulemavu wa Akili katika jamii zetu ni kundi ambalo limesahaulika sana katika maeneo mbalimbali kwenye jamii yetu.
Asanteni kwa kusoma makala yetu hii tuliyotoa tarehe 02.12.2025 kuelekea tarehe 03.12.2025, na Mungu awabariki sana wapendwa endelea kushika mkono shughuli zetu kupitia account zetu.


Hakuna maoni:
Chapisha Maoni